Ufunuo 13:4-14 Biblia Habari Njema (BHN)

4. Watu wote wakaliabudu lile joka kwa sababu lilimpa huyo mnyama uwezo wake. Wakamwabudu pia huyo mnyama wakisema, “Nani aliye kama huyu mnyama? Ni nani awezaye kupigana naye?”

5. Kisha huyo mnyama akaruhusiwa kusema maneno ya kujigamba na kumkufuru Mungu; akaruhusiwa kuwa na mamlaka kwa muda wa miezi arubaini na miwili.

6. Basi, akaanza kumtukana Mungu, kulitukana jina lake, makao yake, na wote wakaao mbinguni.

7. Aliruhusiwa kuwapiga vita na kuwashinda watu wa Mungu. Alipewa mamlaka juu ya watu wa kila kabila, ukoo, lugha na taifa.

8. Wote waishio duniani watamwabudu isipokuwa tu wale ambao majina yao yameandikwa tangu mwanzo wa ulimwengu katika kitabu cha uhai cha Mwanakondoo aliyechinjwa.

9. Aliye na masikio, na asikie!

10. Aliyepangiwa kuchukuliwa mateka lazima atatekwa;wa kuuawa kwa upanga atauawa kwa upanga.Hivyo, watu wa Mungu na wawe na uvumilivu na imani.

11. Kisha, nikamwona mnyama mwingine anatoka ardhini. Alikuwa na pembe mbili kama pembe za kondoo, na aliongea kama joka.

12. Alikuwa na mamlaka kamili kutoka kwa yule mnyama wa kwanza, na akautumia uwezo huo mbele ya huyo mnyama. Akailazimisha dunia yote na wote waliomo humo kumwabudu huyo mnyama wa kwanza ambaye alikuwa na jeraha la kifo lililokuwa limepona.

13. Basi, huyu mnyama wa pili akafanya miujiza mikubwa hata akasababisha moto kutoka mbinguni ushuke duniani mbele ya watu.

14. Aliwapotosha wakazi wa dunia kwa miujiza hiyo aliyojaliwa kutenda mbele ya mnyama wa kwanza. Aliwaambia wakazi wa dunia watengeneze sanamu kwa heshima ya yule mnyama aliyekuwa amejeruhiwa kwa upanga lakini akaishi tena.

Ufunuo 13