Nehemia 3:13-30 Biblia Habari Njema (BHN)

13. Lango la Bondeni lilijengwa upya na Hanuni pamoja na wakazi wa mji wa Zanoa. Wakayaweka malango mahali pake, wakatia bawaba na makomeo yake. Waliujenga upya ukuta ukiwa na urefu wa mita 400 hivi hadi Lango la Samadi.

14. Lango la Samadi lilijengwa upya na Malkiya, mwana wa Rekabu, mkuu wa wilaya ya Beth-hakeremu. Akaliweka lango mahali pake, akatia bawaba na makomeo yake.

15. Lango la Chemchemi lilijengwa upya na Shalumu, mwana wa Kolhoze, mkuu wa wilaya ya Mizpa. Akalifunika, akaliweka lango mahali pake, akatia bawabu na makomeo yake. Kwenye Bwawa la Shela akajenga ukuta ulio karibu na bustani ya kifalme hadi ngazi zinazoshuka toka mji wa mfalme Daudi.

16. Sehemu inayofuata hadi kwenye makaburi ya Daudi, bwawa na majengo ya jeshi ilijengwa upya na Nehemia, mwana wa Azbuki, mkuu wa nusu ya wilaya ya Beth-suri.

17. Baada ya hao, Walawi waliendeleza ujenzi mpya wa ukuta. Sehemu inayofuata ilijengwa upya na Rehumu, mwana wa Bani, na Hashabia, mkuu wa nusu ya wilaya ya Keila, alijenga upya sehemu inayohusu wilaya yake.

18. Baada ya huyo, sehemu zinazofuata zilijengwa upya na ndugu zao. Sehemu inayofuata ilijengwa upya na Bavai, mwana wa Henadadi, mkuu wa nusu ya wilaya ya Keila.

19. Sehemu inayofuata inayoelekeana na ghala ya silaha kwenye pembe ya ukuta ilijengwa upya na Ezeri, mwana wa Yeshua, mkuu wa Mizpa.

20. Sehemu inayofuata tangu pembeni hadi kwenye mlango wa Eliashibu, kuhani mkuu, ilijengwa upya na Baruku, mwana wa Zabai.

21. Sehemu inayofuata tangu mlangoni mwa nyumba ya Eliashibu, kuhani mkuu, hadi mwisho wa nyumba hiyo, ilijengwa upya na Meremothi, mwana wa Uria, mwana wa Hakosi.

22. Sehemu inayofuata ilijengwa upya na makuhani waliokaa katika sehemu tambarare.

23. Benyamini na Hashubu walijenga upya sehemu inayokabiliana na nyumba yake. Azaria, mwana wa Maaseya, mwana wa Anania, alijenga upya sehemu inayokabiliana na nyumba yao.

24. Kuanzia kwenye nyumba ya Azaria hadi pembeni mwa ukuta ilijengwa upya na Binui, mwana wa Henadadi.

25. Sehemu inayofuata, tokea pembeni mwa ukuta na mnara wa ikulu ya juu karibu na uwanda wa ulinzi ilijengwa upya na Palali, mwana wa Uzai. Pedaia, mwana wa Paroshi,

26. akishirikiana na watumishi wa hekalu waliokaa Ofeli, walijenga upya sehemu inayokabiliana na Lango la Maji, upande wa mashariki na mnara mrefu.

27. Sehemu nyingine inayofuata, ikitokea kwenye mnara mrefu hadi ukuta wa Ofeli ilijengwa upya na wakazi wa mji wa Tekoa.

28. Juu ya Lango la Farasi palijawa na makuhani, kila mmoja alijenga sehemu inayokabiliana na nyumba yake.

29. Sadoki, mwana wa Imeri alijenga upya sehemu inayokabiliana na nyumba yake. Sehemu inayofuata, ilijengwa upya na Shemaya, mwana wa Shekania, mlinzi wa Lango la Mashariki.

30. Sehemu inayofuata ikiwa ni sehemu yao ya pili ilijengwa upya na Hanania mwana wa Shelemia, akishirikiana na Hanuni, mwana wa sita wa Zalafu. Meshulamu, mwana wa Berekia, alijenga upya sehemu inayokabiliana na chumba chake.

Nehemia 3