Nehemia 13:21-31 Biblia Habari Njema (BHN)

21. Niliwaonya na kuwaambia: “Hakuna maana kulala nje ya mji. Mkijaribu tena nitatumia nguvu.” Hivyo tangu wakati huo hawakurudi tena siku ya Sabato.

22. Niliagiza Walawi kujitakasa na kwenda kuyalinda malango ili kutunza Sabato iwe takatifu.Ee, Mungu wangu, nikumbuke hata na kwa hili pia na unihurumie kutokana na fadhili zako kuu.

23. Tena wakati huo niliona Wayahudi waliooa wanawake kutoka Ashdodi, Amoni na Moabu;

24. na nusu ya watoto wao walizungumza Kiashdodi au lugha nyingine na hawakuweza kuzungumza lugha ya Yuda.

25. Niliwakemea na kuwaapiza, hata nikawapiga baadhi yao na kuwavuta nywele zao. Niliwalazimisha kuapa kwa jina la Mungu, nikisema, “Binti zenu msiwaoze kwa vijana wao, wala binti zao wasiolewe na vijana wenu au na nyinyi wenyewe.

26. Je, Solomoni hakutenda dhambi kwa sababu ya wanawake wa namna hiyo? Yeye alikuwa mfalme mkuu kuliko wafalme wa mataifa mengine. Mungu alimpenda na akamfanya kuwa mfalme juu ya watu wote wa Israeli, hata hivyo wanawake wa mataifa mengine, walimfanya hata yeye atende dhambi.

27. Je, sasa tufuate mfano wenu na tutende dhambi hii kubwa ya kutomtii Mungu wetu kwa kuoa wanawake wa kigeni?”

28. Mmoja kati ya wana wa Yoyada, mwana wa kuhani mkuu Eliashibu, alioa binti Sanbalati kutoka mji wa Beth-horoni; kwa sababu hiyo nilimfukuza kutoka mbele yangu.

29. Ee Mungu, kumbuka jinsi watu walivyochafua ukuhani na agano la kikuhani na la Walawi.

30. Niliwatakasa watu kutokana na chochote kilichokuwa cha kigeni. Nikatayarisha mwongozo kwa ajili ya makuhani na Walawi kuhusu kazi ya kila mmoja wao.

31. Niliagiza matoleo ya kuni kufanyika katika wakati unaopaswa na malimbuko wakati wake. Ee Mungu wangu, nikumbuke kwa ajili ya haya yote na unijalie mema.

Nehemia 13