5. Mwenyezi-Mungu alipoona wingi wa uovu wa binadamu duniani, na kwamba kila analokusudia binadamu moyoni mwake ni ovu daima,
6. Mwenyezi-Mungu alisikitika sana kwa kumuumba binadamu duniani. Mwenyezi-Mungu alihuzunika sana moyoni mwake,
7. hivyo akasema, “Nitamfuta kabisa duniani binadamu niliyemuumba; nitafutilia mbali pia wanyama wa porini, viumbe vitambaavyo na ndege wa angani. Ninasikitika kwamba niliwaumba duniani.”
8. Lakini Noa alipata fadhili mbele ya Mwenyezi-Mungu.
9. Ifuatayo ni habari juu ya Noa ambaye alikuwa ndiye mwadilifu pekee na ambaye hakuwa na lawama nyakati zake. Alikuwa mcha Mungu.
10. Noa alikuwa na watoto watatu wa kiume: Shemu, Hamu na Yafethi.
11. Mungu aliiona dunia kuwa imeharibika na kujaa ukatili.
12. Naam, Mungu aliiangalia dunia, akaona kuwa imeharibika kabisa, kwa maana kila mtu alifuata njia yake mbovu.
13. Mungu akamwambia Noa, “Nimeamua kuwaangamiza binadamu wote kwa sababu wameijaza dunia ukatili. Naam, nitawaangamiza kabisa pamoja na dunia!