Mwanzo 32:14-31 Biblia Habari Njema (BHN)

14. Mbuzi majike 200 na mabeberu 20, kondoo majike 200 na madume 20,

15. ngamia 30 wanyonyeshao pamoja na ndama wao, ng'ombe majike 40 na mafahali kumi, na punda majike 20 na madume kumi.

16. Akawakabidhi watumishi wake, kila mmoja kundi lake, akawaambia, “Nitangulieni mkiacha nafasi kati ya kundi na kundi katika msafara wenu.”

17. Akamwagiza yule aliyetangulia, “Ndugu yangu Esau atakapokutana nawe na kukuuliza, ‘Wewe ni mtumishi wa nani? Unakwenda wapi? Na wanyama hawa ni wa nani?’

18. Wewe utamjibu, ‘Hii ni mali ya mtumishi wako Yakobo, nayo ni zawadi yako wewe bwana wangu Esau. Tena Yakobo mwenyewe yuko nyuma anafuata.’”

19. Akatoa agizo hilohilo kwa mtumishi wa kundi la pili na la tatu na wengine wote, akisema, “Mtamwambia Esau maneno hayohayo mtakapokutana naye.

20. Zaidi ya yote, mtamwambia, ‘Mtumishi wako Yakobo yuko nyuma, anafuata.’” Yakobo alifanya hivyo akifikiri, “Pengine nitamtuliza kwa zawadi hizi ninazomtangulizia, na baadaye naweza kuonana naye ana kwa ana; huenda atanipokea.”

21. Basi, akatanguliza zawadi zake, lakini yeye mwenyewe akalala kambini usiku huo.

22. Usiku huohuo Yakobo akaamka, akawachukua wake zake wawili, wajakazi wake wawili na watoto wake kumi na mmoja, akapita kivuko cha Yaboki.

23. Baada ya kuwavusha ngambo ya kijito wale waliokuwa nao na mali yake yote,

24. Yakobo alibaki peke yake. Mtu mmoja akaja, akapigana naye mwereka mpaka alfajiri.

25. Mtu huyo alipoona kwamba hawezi kumshinda Yakobo, alimgusa Yakobo nyonga ya kiuno, naye akateguka alipokuwa anapigana naye mwereka.

26. Kisha yule mtu akamwambia Yakobo, “Niache niende zangu, kwani kunapambazuka.” Lakini Yakobo akamwambia, “Sikuachi kamwe, mpaka umenibariki!”

27. Naye akamwuliza, “Jina lako nani?” Yeye akamjibu, “Yakobo.”

28. Yule mtu akamwambia, “Hutaitwa Yakobo tena, bali Israeli, kwa kuwa umeshindana na Mungu na wanadamu, ukashinda.”

29. Ndipo Yakobo akamwambia, “Tafadhali, nakuomba uniambie jina lako.” Lakini yeye akamwambia, “Ya nini kuniuliza jina langu?” Kisha akambariki Yakobo.

30. Yakobo akapaita mahali hapo Penueli, akisema, “Nimemwona Mungu uso kwa uso, nami sikufa.”

31. Jua lilikuwa limekwisha chomoza wakati Yakobo alipoondoka Penueli; akawa anachechemea kwa sababu ya kiuno chake.

Mwanzo 32