1. Baadaye palitokea njaa nchini humo, njaa tofauti na ile ya hapo awali wakati wa uhai wa Abrahamu. Isaka akaenda Gerari kwa Abimeleki mfalme wa Wafilisti.
2. Mwenyezi-Mungu akamtokea Isaka na kumwambia, “Usiende Misri, bali kaa katika nchi nitakayokuambia.
3. Kaa ugenini katika nchi hiyo, nami nitakuwa nawe na kukubariki. Nitatimiza ahadi niliyompa baba yako Abrahamu, kwani nitakupa wewe na wazawa wako nchi hizi zote.
4. Nitawazidisha wazawa wako wawe kama nyota za mbinguni na kuwapa nchi hizi zote. Kutokana na wazawa wako, mataifa yote duniani yatabarikiwa,
5. kwa sababu Abrahamu alinitii mimi, akazingatia maagizo yangu, amri zangu, masharti yangu na sheria zangu.”
6. Basi, Isaka akakaa huko Gerari.
7. Watu wa huko walipomwuliza habari za mkewe, yeye alijibu, “Huyu ni dada yangu.” Aliogopa kusema kwamba ni mke wake kwa kuogopa kwamba wakazi wa nchi wangemuua kwa sababu ya Rebeka, maana Rebeka alikuwa mzuri sana.
8. Baada ya kukaa huko kwa muda mrefu, Abimeleki mfalme wa Wafilisti alichungulia dirishani akamwona Isaka akimkumbatia mkewe Rebeka.
9. Abimeleki akamwita Isaka na kumwambia, “Kumbe huyo ni mke wako! Mbona ulisema ni dada yako?” Isaka akajibu, “Kwa kuwa niliogopa kwamba ningeuawa kwa sababu yake.”
10. Abimeleki akamwuliza, “Ni jambo gani hili ulilotutendea? Mmoja wa watu wangu angaliweza kulala na mkeo bila wasiwasi, nawe ungekuwa umetutia hatiani.”
11. Ndipo Abimeleki akawaonya watu wote akisema, “Yeyote atakayemgusa mtu huyu au mke wake, atauawa.”
12. Mwaka huo Isaka alipanda mbegu katika nchi ile, akavuna mara mia zaidi, maana Mwenyezi-Mungu alimbariki,
13. naye akatajirika. Alizidi kupata mali hadi akawa tajiri sana.
14. Alikuwa na makundi ya kondoo, ng'ombe na watumwa wengi, hata Wafilisti wakamwonea wivu.
15. Wafilisti walikuwa wamevifukia visima vyote vya maji ambavyo watumishi wa Abrahamu, baba yake, walikuwa wamechimba wakati alipokuwa bado hai.
16. Ndipo Abimeleki akamwambia Isaka, “Ondoka kwetu, kwani wewe umetuzidi nguvu.”