13. Hapo Mwenyezi-Mungu akamwuliza Abrahamu, “Kwa nini Sara amecheka na kujiuliza kama kweli itawezekana apate mtoto akiwa mzee?
14. Je, kuna jambo lolote lisilowezekana kwa Mwenyezi-Mungu? Nitakurudia wakati uliopangwa, wakati kama huu mwakani, na Sara atakuwa na mtoto wa kiume.”
15. Lakini Sara, akiwa na hofu, akakana akisema, “Sikucheka!” Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Sivyo! Kucheka, ulicheka.”
16. Ndipo wale watu wakaondoka, wakafika mahali walipoweza kuona mji wa Sodoma; naye Abrahamu akawasindikiza.
17. Basi, Mwenyezi-Mungu akawaza: Je, nimfiche Abrahamu jambo ambalo nimepanga kutenda?
18. Yeye atakuwa baba wa taifa kubwa na kwake mataifa yote ya ulimwengu yatabarikiwa!
19. Nimemchagua yeye na wazawa wake. Yeye atawafunza wazawa wake kushika njia yangu: Wawe waadilifu na wenye kutenda mambo ya haki, nami nipate kuwatimizia ahadi zangu.
20. Basi, Mwenyezi-Mungu akasema, “Kuna malalamiko mengi dhidi ya watu wa Sodoma na Gomora, na dhambi yao ni kubwa mno.
21. Hivyo nitashuka kwenda huko nijionee mwenyewe kama kweli wamefanya kadiri ya kilio kilichonifikia. Nataka kujua.”
22. Kutoka hapo, wale watu wakashika njia kuelekea Sodoma, lakini Mwenyezi-Mungu akawa amebaki, amesimama pamoja na Abrahamu.
23. Basi, Abrahamu akamkaribia Mwenyezi-Mungu, akamwuliza, “Je, kweli utawaangamiza watu wema pamoja na waovu?
24. Huenda ikawa mna watu wema hamsini humo mjini. Je, utauangamiza mji mzima badala ya kuuacha kwa sababu ya hao wema hamsini waliomo humo?
25. Sidhani kama utafanya hivyo! Kuwaua watu wema pamoja na waovu; wema kutendewa sawa na waovu! La, hasha! Hakimu wa dunia yote hataacha kutenda yaliyo sawa!”
26. Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Nikikuta watu wema hamsini kule mjini Sodoma, basi nitauacha mji wote salama kwa ajili yao.”