13. Hapo Mwenyezi-Mungu akamwuliza Abrahamu, “Kwa nini Sara amecheka na kujiuliza kama kweli itawezekana apate mtoto akiwa mzee?
14. Je, kuna jambo lolote lisilowezekana kwa Mwenyezi-Mungu? Nitakurudia wakati uliopangwa, wakati kama huu mwakani, na Sara atakuwa na mtoto wa kiume.”
15. Lakini Sara, akiwa na hofu, akakana akisema, “Sikucheka!” Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Sivyo! Kucheka, ulicheka.”
16. Ndipo wale watu wakaondoka, wakafika mahali walipoweza kuona mji wa Sodoma; naye Abrahamu akawasindikiza.
17. Basi, Mwenyezi-Mungu akawaza: Je, nimfiche Abrahamu jambo ambalo nimepanga kutenda?
18. Yeye atakuwa baba wa taifa kubwa na kwake mataifa yote ya ulimwengu yatabarikiwa!
19. Nimemchagua yeye na wazawa wake. Yeye atawafunza wazawa wake kushika njia yangu: Wawe waadilifu na wenye kutenda mambo ya haki, nami nipate kuwatimizia ahadi zangu.
20. Basi, Mwenyezi-Mungu akasema, “Kuna malalamiko mengi dhidi ya watu wa Sodoma na Gomora, na dhambi yao ni kubwa mno.
21. Hivyo nitashuka kwenda huko nijionee mwenyewe kama kweli wamefanya kadiri ya kilio kilichonifikia. Nataka kujua.”
22. Kutoka hapo, wale watu wakashika njia kuelekea Sodoma, lakini Mwenyezi-Mungu akawa amebaki, amesimama pamoja na Abrahamu.