Methali 27:10-21 Biblia Habari Njema (BHN)

10. Usisahau rafiki zako wala wa baba yako.Ukipatwa na janga usikimbilie kwa nduguyo;afadhali jirani aliye karibu kuliko ndugu aliye mbali.

11. Uwe na hekima mwanangu upate kunifurahisha moyo,nami sitakosa la kumjibu yeyote anayenilaumu.

12. Mwenye busara huona hatari akajificha,lakini mjinga hujitokeza mbele akaumia.

13. Mtu akiahidi mbele yako kumdhamini mgeni, chukua nguo yake;mfanye awajibike kwa kuwadhamini wageni.

14. Amwamkiaye jirani kwa kelele alfajiri,itaeleweka kwamba amemtakia laana.

15. Mke mgomvi daima,ni sawa na tonatona ya maji siku ya mvua.

16. Kumzuia ni sawa na kuzuia upepo,au kukamata mafuta kwa mkono.

17. Chuma hunoa chuma,kadhalika mtu hufundishwa na wenzake.

18. Anayeutunza mtini hula tini,anayemhudumia bwana wake ataheshimiwa.

19. Kama uso ujionavyo wenyewe majini,ndivyo ujijuavyo mwenyewe moyoni.

20. Kuzimu na Uharibifu kamwe havishibi,kadhalika na macho ya watu hayashibi.

21. Ubora wa fedha au dhahabu hupimwa kwa moto,na mtu hupimwa kutokana na sifa zake.

Methali 27