Methali 17:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Afadhali mkate mkavu kwa amani,kuliko karamu katika nyumba ya ugomvi.

2. Mtumwa mwenye busara atachukua nafasi ya mwana mpumbavu,atapata sehemu ya urithi wa jamaa hiyo.

3. Ubora wa dhahabu ama fedha hupimwa kwa moto,lakini Mwenyezi-Mungu ndiye apimaye mioyo ya watu.

4. Mtenda maovu husikiliza maneno mabaya,mwongo hutegea sikio ulimi mdanganyifu.

5. Anayemdhihaki maskini anamtukana Muumba wake;anayefurahia maafa hatakosa kuadhibiwa.

6. Wazee huwaonea fahari wajukuu zao;watoto huwaonea fahari wazazi wao.

7. Maneno mazuri si kawaida kinywani mwa mpumbavu,sembuse maneno ya uongo kinywani mwa kiongozi!

8. Kwa mhongaji, hongo ni kama hirizi;kila afanyacho hufanikiwa.

9. Anayesamehe makosa hujenga urafiki,lakini anayekumbusha makosa hutenga rafiki.

10. Onyo kwa mwenye busara lina maana,kuliko mapigo mia kwa mpumbavu.

11. Afanyalo mtu mwovu ni kuasi tu;mjumbe mkatili atatumwa dhidi yake.

Methali 17