1. Hizi ni methali za Solomoni:Mtoto mwenye hekima ni furaha ya baba yake;lakini mtoto mpumbavu ni huzuni ya mama yake.
2. Mali iliyopatikana kwa njia mbaya haifai,lakini uadilifu huokoa mtu kutoka kifoni.
3. Mwenyezi-Mungu hawaachi waadilifu wapate njaa,lakini huzipinga tamaa za waovu.
4. Uvivu husababisha umaskini,lakini mkono wa mtu wa bidii hutajirisha.
5. Mwenye busara hukusanya wakati wa mavuno,kulala wakati wa kuvuna ni aibu.
6. Mwadilifu hujiletea baraka yeye mwenyewe,lakini kinywa cha mwovu kimesongwa na ukatili.
7. Waadilifu hukumbukwa kwa baraka,lakini waovu watasahaulika kabisa.
8. Mwenye hekima moyoni hutii amri,lakini mpumbavu aropokaye ataangamia.