24. akasema, “Ondokeni hapa! Msichana huyu hakufa, amelala tu.” Nao wakamcheka.
25. Basi, umati wa watu ulipoondolewa, Yesu aliingia ndani, akamshika huyo msichana mkono, naye akasimama.
26. Habari hiyo ikavuma sana katika nchi ile yote.
27. Yesu aliondoka hapo, na alipokuwa anakwenda, vipofu wawili walimfuata wakipiga kelele, “Mwana wa Daudi, utuhurumie!”
28. Yesu alipoingia nyumbani, watu hao wawili wakamwendea, naye akawauliza, “Je, mnaamini kwamba naweza kuwafanyia jambo hilo?” Nao wakamjibu, “Naam, Bwana.”
29. Hapo Yesu akayagusa macho yao, akasema, “Na iwe kwenu kama mnavyoamini.”
30. Macho yao yakafunguliwa. Naye Yesu akawaonya kwa ukali: “Msimwambie mtu yeyote jambo hili.”
31. Lakini wao wakaondoka, wakaeneza habari za Yesu katika nchi ile yote.
32. Watu walipokuwa wanakwenda zao, wengine walimletea Yesu mtu mmoja aliyekuwa bubu kwa sababu alikuwa amepagawa na pepo.
33. Mara tu huyo pepo alipotolewa, mtu huyo aliyekuwa bubu akaanza kuongea tena. Watu wakashangaa na kusema, “Jambo kama hili halijapata kuonekana katika Israeli!”
34. Lakini Mafarisayo wakawa wanasema, “Anawafukuza pepo kwa nguvu ya mkuu wa pepo wabaya.”