12. “Yote mnayotaka watu wawatendee nyinyi, watendeeni wao vivyo hivyo. Hii ndiyo maana ya sheria ya Mose na mafundisho ya manabii.
13. “Ingieni kwa kupitia mlango mwembamba. Kwa maana njia inayoongoza kwenye maangamizi ni pana, na mlango wa kuingilia humo ni mpana; waendao njia hiyo ni wengi.
14. Lakini njia inayoongoza kwenye uhai ni nyembamba, na mlango wa kuingilia humo ni mwembamba; ni watu wachache tu wanaoweza kuigundua njia hiyo.
15. “Jihadharini na manabii wa uongo. Wao huja kwenu wakionekana kama kondoo kwa nje, lakini kwa ndani ni mbwamwitu wakali.
16. Mtawatambua kwa matendo yao. Je, watu huchuma zabibu katika miti ya miiba, au tini katika mbigili? La!
17. Basi, mti mzuri huzaa matunda mazuri, na mti mbaya huzaa matunda mabaya.
18. Mti mzuri hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mbaya hauwezi kuzaa matunda mazuri.
19. Kila mti usiozaa matunda mazuri utakatwa na kutupwa motoni.
20. Kwa hiyo, mtawatambua kwa matendo yao.
21. “Si kila aniambiaye, ‘Bwana, Bwana’, ataingia katika ufalme wa mbinguni; ila ni yule tu anayetimiza matakwa ya Baba yangu aliye mbinguni.
22. Wengi wataniambia siku ile ya hukumu: ‘Bwana, Bwana! Kwa jina lako tulitangaza ujumbe wako, na kwa jina lako tuliwatoa pepo na kufanya miujiza mingi’.
23. Hapo nitawaambia: ‘Sikuwajua nyinyi kamwe; ondokeni mbele yangu, enyi watenda maovu.’
24. “Kwa hiyo, kila mtu anayeyasikia maneno yangu na kuyazingatia, anafanana na mtu mwenye busara, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba.
25. Mvua ikanyesha, mito ikafurika, pepo kali zikavuma na kuipiga nyumba hiyo. Lakini haikuanguka kwa sababu ilikuwa imejengwa juu ya mwamba.
26. “Lakini yeyote anayesikia maneno yangu haya bila kuyazingatia, anafanana na mtu mpumbavu aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga.
27. Mvua ikanyesha, mito ikafurika, pepo kali zikavuma na kuipiga nyumba hiyo, nayo ikaanguka; tena anguko hilo lilikuwa kubwa.”
28. Yesu alipomaliza kusema maneno hayo, umati wa watu ukashangazwa na mafundisho yake.