15. “Ole wenu waalimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnasafiri baharini na nchi kavu ili kumpata mtu mmoja afuate dini yenu. Mnapompata, mnamfanya astahili maradufu kwenda katika moto wa Jehanamu kuliko nyinyi wenyewe.
16. “Ole wenu viongozi vipofu! Nyinyi mwasema ati mtu akiapa kwa hekalu, kiapo hicho si kitu; lakini akiapa kwa dhahabu ya hekalu, kiapo hicho kinamshika.
17. Enyi vipofu wapumbavu! Kipi kilicho cha maana zaidi: Dhahabu au hekalu linalofanya hiyo dhahabu kuwa takatifu?
18. Tena mwasema ati mtu akiapa kwa madhabahu si kitu; lakini akiapa kwa zawadi iliyowekwa juu ya madhabahu, kiapo hicho humshika.
19. Enyi vipofu! Ni kipi kilicho cha maana zaidi: Ile zawadi, au madhabahu ambayo hufanya hiyo zawadi kuwa takatifu?