25. Hivyo Yesu akawaita, akawaambia, “Mnajua kwamba watawala wa mataifa hutawala watu wao kwa mabavu, na wakuu hao huwamiliki watu wao.
26. Lakini kwenu isiwe hivyo, ila anayetaka kuwa mkuu kati yenu sharti awe mtumishi wa wote;
27. na anayetaka kuwa wa kwanza kati yenu sharti awe mtumishi wenu.
28. Jinsi hiyohiyo, Mwana wa Mtu hakuja kutumikiwa, bali kutumikia na kutoa maisha yake kuwa fidia ya watu wengi.”
29. Yesu alipokuwa anaondoka mjini Yeriko, umati wa watu ulimfuata.
30. Basi, kulikuwa na vipofu wawili wameketi kando ya njia, na waliposikia kwamba Yesu alikuwa anapitia hapo, walipaza sauti: “Bwana, Mwana wa Daudi, utuhurumie!”
31. Ule umati wa watu ukawakemea na kuwaambia wanyamaze. Lakini wao wakazidi kupaza sauti: “Bwana, Mwana wa Daudi, utuhurumie!”
32. Yesu akasimama, akawaita na kuwauliza, “Mnataka niwafanyie nini?”
33. Wakamjibu, “Bwana, tunaomba macho yetu yafumbuliwe.”
34. Basi, Yesu akawaonea huruma, akawagusa macho yao, na papo hapo wakaweza kuona, wakamfuata.