Mathayo 17:7-17 Biblia Habari Njema (BHN)

7. Yesu akawaendea, akawagusa, akasema, “Simameni, msiogope!”

8. Walipoangalia juu hawakumwona mtu, ila Yesu peke yake.

9. Basi, walipokuwa wanashuka mlimani, Yesu akawaonya: “Msimwambie mtu mambo mliyoyaona mpaka Mwana wa Mtu atakapofufuliwa kutoka wafu.”

10. Kisha wanafunzi wakamwuliza, “Mbona waalimu wa sheria wanasema ni lazima kwanza Elia aje?”

11. Yesu akawajibu, “Kweli, Elia atakuja kutayarisha mambo yote.

12. Lakini nawaambieni, Elia amekwisha kuja nao hawakumtambua, bali walimtendea jinsi walivyotaka. Mwana wa Mtu atateswa vivyo hivyo mikononi mwao.”

13. Hapo hao wanafunzi wakafahamu kwamba alikuwa akiwaambia juu ya Yohane Mbatizaji.

14. Walipoufikia tena ule umati wa watu, mtu mmoja alimwendea Yesu, akampigia magoti,

15. akasema, “Bwana, mwonee huruma mwanangu kwa kuwa ana kifafa, tena anateseka sana; mara nyingi yeye huanguka motoni na majini.

16. Nilimleta kwa wanafunzi wako lakini hawakuweza kumponya.”

17. Yesu akajibu, “Enyi kizazi kisicho na imani, kilichopotoka! Nitakaa nanyi mpaka lini? Nitawavumilia nyinyi mpaka lini? Mleteni hapa huyo mtoto.”

Mathayo 17