20. kabla ya kuingia kwenye hema la mkutano au kukaribia madhabahu ili kunitolea tambiko mimi Mwenyezi-Mungu, tambiko zitolewazo kwa moto; watafanya hivyo wasije wakafa.
21. Ni lazima wanawe mikono na miguu yao wasije wakafa. Hii itakuwa ni kanuni kwao daima, tangu Aroni na uzao wake, vizazi hata vizazi.”
22. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose,
23. “Utachukua viungo bora kabisa kama vifuatavyo: Manemane ya maji kilo sita, mdalasini wenye harufu nzuri kilo tatu, miwa yenye harufu nzuri kilo tatu,
24. na aina nyingine ya mdalasini kilo 6 – vipimo hivyo vyote viwe kufuatana na vipimo vya hema takatifu; chukua pia lita 4 za mafuta.
25. Kutokana na viungo hivyo utatengeneza mafuta matakatifu uyachanganye kama afanyavyo fundi wa manukato; hayo yatatumika kuweka vitu wakfu.
26. Kisha utalimiminia mafuta hayo hema la mkutano, na sanduku la maamuzi;
27. meza na vyombo vyake vyote; kinara cha taa na vyombo vyake, madhabahu ya kufukizia ubani,
28. madhabahu ya sadaka za kuteketezwa na vyombo vyake vyote, birika na tako lake.
29. Utaviweka wakfu, ili viwe vitakatifu kabisa. Chochote kitakachovigusa vifaa hivyo, kitakuwa kitakatifu.
30. Kisha mpake mafuta Aroni na wanawe na kuwaweka wakfu ili wanitumikie kama makuhani.
31. Waambie Waisraeli kwamba haya yatakuwa mafuta yangu matakatifu ya kupaka katika vizazi vyenu vyote.
32. Mafuta haya kamwe yasimiminiwe mtu yeyote wa kawaida, wala yasitengenezwe mafuta mengine ya aina hii; haya ni mafuta matakatifu na ni lazima yawe daima matakatifu kwenu.
33. Yeyote atakayetengeneza mafuta kama haya, au kumpaka mtu asiyestahili kupakwa mafuta haya, mtu huyo atatengwa mbali na watu wake.”
34. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Utachukua vipimo vinavyolingana vya viungo vitamu vifuatavyo: Utomvu wa natafi, utomvu wa shekelethi, utomvu wa kelbena na ubani safi.