13. Basi, mnamo wakati wa jioni kukaja kware wengi, wakafunika kambi ya Waisraeli. Asubuhi yake kukatokea umande, ukatanda kandokando ya kambi yao.
14. Umande huo ulipotoweka, kukabaki huko nyikani kitu kama mkate mwembamba na mwepesi.
15. Waisraeli walipoona kitu hicho walishangaa, wakaulizana, “Nini hiki?” Hawakujua kilikuwa kitu gani. Basi, Mose akawaambia, “Huu ni mkate ambao Mwenyezi-Mungu amewapa mle.
16. Mwenyezi-Mungu ameamuru mfanye hivi: Kila mtu na akusanye chakula kiasi anachoweza kula; ataokota kiasi cha pishi moja kwa kila mtu hemani mwake.”
17. Basi, Waisraeli wakafanya hivyo, na ikawa kwamba, wengine waliokota kwa wingi na wengine kidogo.
18. Lakini wote walipokipima kipimo walichookota katika pishi, waligundua kuwa aliyeokota kingi hakuwa na cha ziada, na aliyeokota kidogo, hakupungukiwa. Kila mmoja alikuwa ameokota kiasi alichoweza kula.