37. Waisraeli waliondoka mjini Ramesesi, wakasafiri kwa miguu kuelekea Sukothi. Walikuwa wanaume wapatao 600,000, licha ya wanawake na watoto.
38. Kulikuwa pia na kundi la watu wengine walioandamana nao pamoja na mifugo mingi, kondoo na ng'ombe.
39. Kwa kuwa walikuwa wameondoka Misri kwa haraka, hawakuweza kutayarisha chakula cha safarini, ila tu ule unga uliokandwa bila kutiwa chachu. Basi, wakaoka mikate isiyotiwa chachu.
40. Waisraeli walikuwa wameishi nchini Misri kwa muda wa miaka 430.
41. Katika siku ya mwisho ya mwaka wa 430, siku hiyohiyo maalumu ndipo makabila yote ya Mwenyezi-Mungu yaliondoka nchini Misri.
42. Usiku huo ambao Mwenyezi-Mungu alikesha ili kuwatoa Waisraeli nchini Misri, unapaswa kuadhimishwa na Waisraeli wote na vizazi vyao vyote, kama usiku wa kukesha kwa heshima ya Mwenyezi-Mungu.
43. Mwenyezi-Mungu aliwaambia Mose na Aroni, “Yafuatayo ni maagizo juu ya adhimisho la Pasaka. Mgeni yeyote hatashiriki chakula cha Pasaka.
44. Lakini mtumwa yeyote aliyenunuliwa kwa fedha, baada ya kumtahiri, ataruhusiwa kushiriki.
45. Msafiri yeyote, wala kibarua yeyote, hatashiriki chakula hicho.
46. Mwanakondoo wa Pasaka ataliwa katika nyumba moja. Hamtatoa nyama yoyote nje ya nyumba alimochinjiwa, wala hamtavunja hata mfupa mmoja wa mnyama wa Pasaka.
47. Jumuiya yote ya watu wa Israeli itaadhimisha sikukuu hiyo.
48. Mgeni yeyote anayeishi miongoni mwenu akipenda kuadhimisha sikukuu ya Pasaka, ni lazima kwanza wanaume wote wa nyumba yake watahiriwe; hapo atahesabiwa kuwa kama mwenyeji na kuruhusiwa kushiriki. Mwanamume yeyote asiyetahiriwa asishiriki kamwe.
49. Sheria zilezile zitamhusu mzalendo Mwisraeli na wageni watakaoishi miongoni mwenu”.