18. Basi, mtakula mikate isiyotiwa chachu kuanzia jioni ya siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza, mpaka jioni ya siku ya ishirini na moja ya mwezi huohuo wa kwanza.
19. Katika siku hizo saba, msiwe na chachu yoyote katika nyumba zenu. Mtu yeyote, awe mgeni au mwenyeji, akila kitu kilichotiwa chachu, ataondolewa miongoni mwa jumuiya ya Waisraeli.
20. Popote pale mnapoishi, ni mwiko kabisa kula chochote kilichotiwa chachu. Mnapaswa kula mikate isiyotiwa chachu.”
21. Basi, Mose akawaita wazee wote wa Waisraeli, akawaambia, “Chagueni kila mmoja wenu, kulingana na jamaa yake, mwanakondoo na kumchinja kwa sikukuu ya Pasaka.
22. Mtachukua majani ya husopo na kuyachovya katika damu ndani ya birika na kupaka kwenye vizingiti na miimo yote miwili ya milango ya nyumba zenu. Mtu yeyote asitoke nje ya nyumba usiku huo hadi asubuhi.
23. Maana mimi Mwenyezi-Mungu nitapita kuwaua Wamisri. Lakini nitakapoiona damu iliyopakwa kwenye vizingiti na miimo ya nyumba zenu, nitazipita na wala sitamruhusu mwangamizi kuingia katika nyumba zenu na kuwaua.
24. Shikeni jambo hilo nyinyi na wazawa wenu kama agizo la milele.
25. Mtakapoingia katika nchi ile ambayo mimi Mwenyezi-Mungu nitawapa, kama nilivyoahidi, ni lazima kulitekeleza.
26. Kila wakati watoto wenu watakapowauliza, ‘Jambo hili lina maana gani?’
27. Nyinyi mtawajibu, ‘Hii ni tambiko ya Pasaka kwa heshima ya Mwenyezi-Mungu, kwa sababu alizipita nyumba za Waisraeli nchini Misri alipowaua Wamisri, lakini sisi hakutuua.’” Waisraeli wakainamisha vichwa na kumwabudu Mwenyezi-Mungu.
28. Kisha Waisraeli wakaenda, wakafanya kama walivyoambiwa na Mose na Aroni kulingana na amri ya Mwenyezi-Mungu.
29. Mnamo usiku wa manane, Mwenyezi-Mungu aliwaua wazaliwa wa kwanza wote wa Misri. Wote walikufa, tangu mzaliwa wa kwanza wa Farao, mrithi wa ufalme, hadi mzaliwa wa kwanza wa mfungwa gerezani. Hata wazaliwa wa kwanza wa wanyama nao walikufa.
30. Basi Farao, watumishi wake na wakazi wote wa Misri wakaamka usiku. Kukawa na kilio kikubwa nchini kote Misri kwa maana hapakuwa hata nyumba moja ambamo hakufa mtu.
31. Hapo Farao akawaita Mose na Aroni, usiku huohuo, akamwambia, “Amkeni! Ondokeni miongoni mwa watu wangu. Nendeni, nyinyi pamoja na hao Waisraeli, mkamtumikie Mwenyezi-Mungu kama mlivyosema.
32. Chukueni makundi yenu ya kondoo na ng'ombe, mwondoke; niombeeni na mimi baraka.”
33. Wamisri wakawahimiza Waisraeli waondoke haraka, wakisema, “Hakika tutakufa sote!”
34. Basi, Waisraeli wakauchukua unga wao uliokandwa kabla haujatiwa chachu, na mabakuli yao ya kukandia wakiwa wamezifunga kwa nguo na kubeba mabegani.
35. Waisraeli walikuwa wamekwisha fanya kama Mose alivyowaagiza hapo awali: Waliwaomba Wamisri wawapatie vito vya fedha, dhahabu na mavazi.
36. Naye Mwenyezi-Mungu alikwisha wafanya Waisraeli wapendwe na Wamisri, nao Wamisri wakawapa kila kitu walichoomba. Ndivyo Waisraeli walivyowapokonya Wamisri mali yao.