Kumbukumbu La Sheria 3:21-29 Biblia Habari Njema (BHN)

21. “Kisha nikamwamuru Yoshua, ‘Wewe umeona kwa macho yako mambo yote ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, amewatendea wafalme hawa wawili, Sihoni na Ogu; basi, yeye atawatendea vivyo hivyo wafalme wa nchi zote mtakazopitia.

22. Msiwaogope maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ndiye atakayepigana kwa ajili yenu.’

23. “Wakati huo nilimsihi Mwenyezi-Mungu nikisema,

24. ‘Ee Bwana, Mwenyezi-Mungu, ninajua umenionesha mimi mtumishi wako mwanzo tu wa ukuu wako na uwezo wako. Maana, kuna mungu gani huko mbinguni au duniani awezaye kufanya mambo makuu na ya ajabu kama ulivyofanya wewe?

25. Nakuomba nivuke mto Yordani, niione nchi hiyo nzuri magharibi ya Yordani; naam, nchi nzuri ya kupendeza ya milima, pamoja na milima ya Lebanoni’.

26. “Lakini Mwenyezi-Mungu alinikasirikia kwa sababu yenu, akakataa kunisikiliza. Badala yake aliniambia, ‘Inatosha! Usiseme tena jambo hili.

27. Panda mpaka kilele cha mlima Pisga, utazame vizuri upande wa magharibi, kaskazini, kusini na mashariki, na kuiona nchi hiyo; ila wewe hutavuka huu mto wa Yordani.

28. Lakini mpe Yoshua maagizo, umtie moyo na kumuimarisha, maana yeye ndiye atakayewaongoza watu hawa hadi ngambo, kuimiliki nchi utakayoiona’.

29. “Basi, tukabaki hapa bondeni mbele ya Beth-peori.”

Kumbukumbu La Sheria 3