1. “Akitokea nabii au mtabiri wa ndoto miongoni mwenu, akawaahidi na kuwapa ishara au maajabu fulani,
2. halafu ishara au maajabu hayo yatokee, kisha aseme: ‘Tufuate miungu mingine na kuitumikia, (miungu ambayo hamjapata kuijua)’,
3. msisikilize maneno yake nabii huyo au mtabiri wa ndoto, kwa maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu anawatumia wao kuwajaribu, ili ajue kama mnampenda yeye Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kwa moyo wenu wote na kwa roho yenu yote.
4. Mfuateni na kumcha Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na kushika amri zake na kuitii sauti yake; mtumikieni na kuambatana naye.
5. Lakini nabii huyo au mtabiri wa ndoto atauawa, kwa sababu atakuwa amewafundisha uasi dhidi ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliyewatoa katika nchi ya Misri na kuwakomboa kutoka utumwani, ili muiache njia ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu aliwaamuru muifuatea. Hivyo ndivyo mtakavyokomesha uovu miongoni mwenu.
6. “Ikiwa ndugu yako wa tumbo moja, au mtoto wako wa kiume au wa kike, au mke wako umpendaye sana, au rafiki yako mwandani, atakushawishi kwa siri akisema, ‘Twende tukaabudu miungu mingine’, miungu ambayo wewe wala babu zenu hamuijui,
7. au baadhi ya miungu ya watu wanaoishi karibu nanyi, au miungu ya watu waishio mbali toka ncha moja ya dunia hadi nyingine,
8. usikubali kushawishiwa, wala usimsikilize au kumhurumia, wala usimwachilie wala kumficha;
9. bali utamuua. Wewe utakuwa wa kwanza kuchukua hatua ya kumuua, kisha watu wengine wote watafuata.
10. Mpigeni mawe mpaka afe! Kwa sababu amejaribu kukuvutia mbali na Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, aliyekutoa utumwani nchini Misri.
11. Hivyo, Waisraeli wote watasikia na kuogopa, na kamwe hawatafanya uovu kama huo.
12. “Mtakapoishi katika miji ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, anawapa, huenda mkasikia
13. kuwa watu fulani mabaradhuli miongoni mwenu, wamewashawishi watu wa mji wakisema, ‘Twende tukaabudu miungu mingine,’ miungu ambayo bado hamjawahi kuijua,
14. basi mtapeleleza na kufanya uchunguzi na kuuliza kwa makini; na kama ni kweli kuwa jambo la kuchukiza limetendeka kati yenu,