Isaya 36:15-22 Biblia Habari Njema (BHN)

15. Msikubali awashawishi ili mumtegemee Mwenyezi-Mungu akisema, ‘Mwenyezi-Mungu hakika atatuokoa na mji huu hautatiwa mkononi mwa mfalme wa Ashuru.’

16. Msimsikilize Hezekia; maana mfalme wa Ashuru anasema: ‘Muwe na amani nami, na kujisalimisha kwangu. Hapo kila mmoja wenu ataweza kula matunda ya mzabibu wake mwenyewe na ya matunda ya mtini wake mwenyewe na kunywa maji ya kisima chake mwenyewe.

17. Mpaka baadaye nitakapokuja na kuwapelekeni katika nchi kama hii yenu; nchi yenye nafaka na divai, nchi yenye mkate na mashamba ya mizabibu.’

18. Angalieni basi Hezekia asiwahadae akisema kwamba Mwenyezi-Mungu atawaokoeni. Je, kuna yoyote kati ya miungu ya mataifa aliyewahi kuokoa nchi yake mkononi mwa mfalme wa Ashuru?

19. Je, iko wapi miungu ya Hamathi na Arpadi? Iko wapi miungu ya Sefarvaimu? Je, imeokoa Samaria mkononi mwangu?

20. Ni nani miongoni mwa miungu ya nchi hizi aliyeokoa nchi zao katika mkono wangu, hata iwe kwamba Mwenyezi-Mungu ataweza kuuokoa mji wa Yerusalemu mkononi mwangu?”

21. Lakini watu walinyamaza, wala hawakumjibu neno kama vile walivyoamriwa na mfalme akisema, “Msimjibu.”

22. Kisha Eliakimu mwana wa Hilkia aliyekuwa mkuu wa ikulu, katibu Shebna, na Yoa mwana wa Asafu mwandishi, wakamwendea mfalme Hezekia huku mavazi yao yakiwa yameraruliwa, wakamweleza maneno ya mkuu wa matowashi.

Isaya 36