Isaya 3:14-26 Biblia Habari Njema (BHN)

14. Mwenyezi-Mungu anawashtakiwazee na wakuu wa watu wake:“Nyinyi ndio mlioliharibu shamba la mizabibu;mali walizowanyanganywa maskini zimo nyumbani kwenu.

15. Mnamaanisha nini kuwakandamiza watu wangu,kuwatendea ukatili watu maskini?Nauliza mimi Bwana, Mwenyezi-Mungu wa majeshi.”

16. Mwenyezi-Mungu asema:“Wanawake wa Siyoni wana kiburi;wanatembea wameinua shingo juu,wakipepesa macho yao kwa tamaa.Hatua zao ni za maringo,na miguuni njuga zinalia.

17. Basi, mimi Mwenyezi-Mungu nitawaadhibu;nitawanyoa nywele hao wanawake wa Siyoni,na kuwavua nguo za kufunika uchi wao.”

18. Siku yaja ambapo Mwenyezi-Mungu atawanyanganya wanawake wa Yerusalemu vitu vyote wanavyoringia: Njuga, kaya, mikufu,

19. vipuli, vikuku, shungi,

20. vitambaa vya kichwani, bangili, vibwebwe, vibweta vya marashi, hirizi,

21. pete, hazama,

22. mavazi ya sikukuu, mitandio, majoho, mikoba,

23. mavazi yaoneshayo, mavazi ya kitani, vilemba na shela.

24. Badala ya kunukia marashi watatoa uvundo;badala ya mishipi mizuri watatumia kamba;badala ya nywele nzuri watakuwa na upara;badala ya mavazi mazuri watavaa matambara;uzuri wao wote utageuka kuwa aibu.

25. Wanaume wenu wataangamia kwa upanga,watu wenu wenye nguvu watakufa vitani.

26. Malango ya mji yatalia na kuomboleza;nao mji utakuwa kama mwanamke aliyepokonywa kila kitu, ameketi mavumbini.

Isaya 3