17. Kisha, atamimina maji matakatifu katika chombo cha udongo na kutwaa vumbi kutoka sakafuni mwa hema takatifu na kuitia katika maji hayo ili kuyafanya machungu.
18. Kuhani atamweka mbele ya Mwenyezi-Mungu na kumfunua nywele na kumpa sadaka hiyo ya nafaka itolewayo kwa sababu ya shuku ya mumewe. Kuhani mwenyewe atashikilia kile chombo chenye maji machungu yaletayo laana.
19. Halafu kuhani atamwapisha mwanamke huyo akisema: ‘Ikiwa hukulala na mwanamume mwingine, ukajitia najisi hali uko chini ya mamlaka ya mumeo, basi, hutapatwa na laana iletwayo na maji haya machungu.
20. Lakini kama umepotoka hali uko chini ya mamlaka ya mumeo, ukajitia najisi kwa kulala na mwanamume mwingine asiye mume wako,
21. Mwenyezi-Mungu na akuadhibu hata uwe laana na apizo miongoni mwa watu wako, uwe tasa na tumbo lako livimbe.
22. Maji haya yaletayo laana na yaingie tumboni mwako na kukufanya tasa na tumbo lako livimbe.’ Naye mwanamke ataitikia, ‘Amina, Amina.’
23. “Kisha kuhani ataandika laana hizi kitabuni na kuzioshea katika maji machungu;
24. naye atamnywesha mwanamke hayo maji machungu yaletayo laana nayo yataingia ndani yake na kumletea maumivu makali;