14. Basi, mumewe akiingiwa na shaka na kuwa na wivu juu ya mkewe aliyejitia najisi; au kama amekuwa na wivu juu ya mke wake ingawa mkewe hakujitia najisi,
15. basi wote wawili watakwenda kwa kuhani na kupeleka sadaka inayotakiwa, yaani sehemu ya kumi ya unga wa shayiri; lakini bila kuitia mafuta au ubani, kwa kuwa ni sadaka ya nafaka ya mume anayemshuku mkewe, sadaka inayotolewa kuhusu kosa ambalo linabainishwa.
16. “Kuhani atampeleka huyo mwanamke karibu, na kumsimamisha mbele ya Mwenyezi-Mungu.
17. Kisha, atamimina maji matakatifu katika chombo cha udongo na kutwaa vumbi kutoka sakafuni mwa hema takatifu na kuitia katika maji hayo ili kuyafanya machungu.
18. Kuhani atamweka mbele ya Mwenyezi-Mungu na kumfunua nywele na kumpa sadaka hiyo ya nafaka itolewayo kwa sababu ya shuku ya mumewe. Kuhani mwenyewe atashikilia kile chombo chenye maji machungu yaletayo laana.
19. Halafu kuhani atamwapisha mwanamke huyo akisema: ‘Ikiwa hukulala na mwanamume mwingine, ukajitia najisi hali uko chini ya mamlaka ya mumeo, basi, hutapatwa na laana iletwayo na maji haya machungu.
20. Lakini kama umepotoka hali uko chini ya mamlaka ya mumeo, ukajitia najisi kwa kulala na mwanamume mwingine asiye mume wako,
21. Mwenyezi-Mungu na akuadhibu hata uwe laana na apizo miongoni mwa watu wako, uwe tasa na tumbo lako livimbe.
22. Maji haya yaletayo laana na yaingie tumboni mwako na kukufanya tasa na tumbo lako livimbe.’ Naye mwanamke ataitikia, ‘Amina, Amina.’
23. “Kisha kuhani ataandika laana hizi kitabuni na kuzioshea katika maji machungu;
24. naye atamnywesha mwanamke hayo maji machungu yaletayo laana nayo yataingia ndani yake na kumletea maumivu makali;
25. kisha kuhani atachukua ile sadaka ya nafaka ya wivu mikononi mwa mwanamke huyo na kuitikisa mbele ya Mwenyezi-Mungu, na kuipeleka madhabahuni.
26. Halafu, atatwaa konzi moja ya sadaka hiyo ya nafaka kwa ukumbusho na kuiteketeza madhabahuni. Hatimaye atamnywesha mwanamke maji hayo.
27. Akisha kunywa, kama amejitia najisi na hakuwa mwaminifu kwa mume wake, maji hayo yaletayo laana yatamletea maumivu makali sana; mwili wake utavimba na tumbo lake la uzazi litaharibika. Mwanamke huyo atakuwa laana miongoni mwa watu wake.