Hesabu 34:4-18 Biblia Habari Njema (BHN)

4. Kisha utapinda kusini kuelekea pito la Akrabimu na kupitia Sini hadi Kadesh-barnea, upande wa kusini. Kutoka hapo, mpaka utapinda kuelekea kaskazini-magharibi hadi Hasar-adari na kupita hadi Azmoni.

5. Kutoka Azmoni utapinda kuelekea kijito cha Misri kwenye mpaka wa Misri na kuishia bahari ya Mediteranea.

6. “Mpaka wenu wa upande wa magharibi utakuwa bahari ya Mediteranea.

7. “Mpaka wenu wa upande wa kaskazini utakuwa kama ifuatavyo: Kutoka bahari ya Mediteranea, mtatia alama hadi Mlima Hori.

8. Kutoka Mlima Hori mtatia alama hadi pito la Hamathi, na kuendelea hadi Sedadi,

9. na kupita hadi Zifroni na kuishia Hazar-enani; huo utakuwa mpaka wenu wa kaskazini.

10. “Mpaka wenu wa upande wa mashariki mtauweka kutoka Hazar-enani hadi Shefamu.

11. Kutoka Shefamu utaelekea kusini hadi Ribla, mashariki mwa Aini; kisha mpaka huo utakwenda chini hadi mteremko wa mashariki wa ziwa Kinerethi,

12. halafu utateremka kufuata mto Yordani hadi Bahari ya Chumvi; hii ndiyo itakuwa nchi yako kama mpaka ulivyo.”

13. Basi, Mose akawaambia Waisraeli, “Hii ndiyo nchi mtakayoirithi kwa kupiga kura, nchi ambayo Mwenyezi-Mungu ameagiza yapewe makabila tisa na nusu.

14. Kabila la Reubeni na la Gadi, na nusu ya kabila la Manase yamepata urithi wao kulingana na koo zao.

15. Makabila hayo mawili na nusu yamepata urithi wao ngambo ya mto Yordani upande wa mashariki, mkabala wa Yeriko, mawioni.”

16. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose,

17. “Kuhani Eleazari na Yoshua mwana wa Nuni ndio watakaowagawia watu nchi kuwa mali yao.

18. Utachukua pia kiongozi mmoja kutoka kila kabila kusaidia katika ugawaji wa nchi.

Hesabu 34