39. Punda wao walikuwa 30,500, na katika hao 61 walitolewa zaka kwa Mwenyezi-Mungu.
40. Watu walikuwa 16,000, na katika hao sehemu ya Mwenyezi-Mungu ilikuwa ni watu thelathini na wawili.
41. Basi, Mose akampa kuhani Eleazari zaka hiyo iliyotolewa kwa Mwenyezi-Mungu, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose.
42. Ile nusu waliopewa Waisraeli, ambayo Mose aliitenga na ile nusu waliyopewa wanajeshi waliokwenda vitani,
43. ilikuwa kondoo 337,500,
44. ng'ombe 36,000,
45. punda 30,500,
46. na watu 16,000.
47. Kutoka nusu hii waliyopewa Waisraeli, Mose alitwaa mmoja kati ya kila mateka hamsini na wanyama hamsini, kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu, akawapa Walawi ambao walihudumu katika hema la Mwenyezi-Mungu.
48. Kisha maofisa wa majeshi, makapteni na makamanda wa askari wakamwendea Mose,
49. wakamwambia “Watumishi wako tumewahesabu askari wote walio chini yetu na tumeona kwamba hakuna hata mmoja wao anayekosekana.
50. Basi, tumeleta vyombo vya dhahabu, vikuku, bangili, pete za mhuri, vipuli na shanga ambavyo kila mtu alipata. Tumevitoa ili nafsi zetu zifanyiwe upatanisho mbele ya Mwenyezi-Mungu.”
51. Mose na kuhani Eleazari wakapokea vitu vyote vilivyonakshiwa kwa dhahabu.
52. Jumla ya dhahabu yote waliyomtolea Mwenyezi-Mungu ilikuwa karibu kilo 200.
53. (Kila askari alijichukulia nyara zake binafsi).
54. Basi, Mose na kuhani Eleazari wakaipokea dhahabu hiyo kutoka kwa makamanda wakaipeleka katika hema la mkutano, iwe ukumbusho wa Waisraeli mbele ya Mwenyezi-Mungu.