10. Lakini jumuiya yote ikatishia kuwapiga mawe. Ghafla, utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukatokea juu ya hema la mkutano, mbele ya Waisraeli wote.
11. Kisha Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Watu hawa watanidharau mpaka lini? Na, mpaka lini wataendelea kutoniamini, hata pamoja na miujiza yote niliyotenda kati yao?
12. Nitawapiga kwa maradhi mabaya na kuwatupilia mbali; lakini, kutokana nawe, nitaunda taifa lingine kubwa, lenye nguvu kuliko wao.”
13. Lakini Mose akamwambia Mwenyezi-Mungu, “Uliwatoa watu hawa nchini Misri kwa nguvu yako. Wamisri watakaposikia kwamba umewatenda hivyo watu wako,
14. watawapasha habari wakazi wa nchi hii. Maana watu hawa wamekwisha pata habari kwamba wewe, ee Mwenyezi-Mungu, u pamoja nasi; maana wewe, ee Mwenyezi-Mungu, unaonekana waziwazi wingu lako linaposimama juu yetu, na kwamba wewe hututangulia mchana kwa nguzo ya wingu na usiku kwa nguzo ya moto.
15. Sasa basi, ukiwaua watu wako wote kwa mara moja, mataifa ambayo yamekwisha sikia sifa zako yatasema,
16. ‘Mwenyezi-Mungu aliwaua watu wake jangwani kwa sababu alishindwa kuwapeleka katika nchi aliyoahidi kuwapa.’