Ezekieli 43:10-20 Biblia Habari Njema (BHN)

10. “Sasa, ewe mtu, waeleze Waisraeli habari za nyumba ya Mungu na wajifunze ramani yake. Waaibike kutokana na machukizo yao waliyotenda.

11. Wakiona aibu kutokana na matendo yao, waeleze ramani ya nyumba ya Mungu: Ramani yake yenyewe, milango ya kuingilia na kutokea, umbo lake lote, mipango ya kila kitu, kanuni zake na masharti yake. Waandikie hayo yote waziwazi ili waweze kuona yote yalivyopangwa na waweze kuzifuata kanuni na masharti yake.

12. Hii ndiyo sheria kuhusu nyumba ya Mwenyezi-Mungu: Eneo lote linalozunguka nyumba ya Mwenyezi-Mungu juu ya mlima lazima liwe takatifu kabisa.”

13. Vipimo vya madhabahu, vitakuwa vilevile kama vipimo vya hekalu. Kuuzunguka msingi wa madhabahu, kutakuwa na mfereji wenye kina cha sentimita 50 na upana wa sentimita 50, pamoja na ukingo wenye kina cha sentimita 25.

14. Sehemu ya madhabahu itakayokuwa chini kabisa tokea juu ya msingi itakuwa na kimo cha mita 1. Sehemu itakayofuata itawekwa nyuma kutoka kwenye ukingo sentimita 50 kuzunguka, na kimo cha mita 2. Sehemu itakayofuata nayo itawekwa nyuma ya ukingo sentimita 50 kuzunguka.

15. Sehemu hii ya juu, ambayo itatumika kuteketezea sadaka, itakuwa mraba, kila upande mita 2. Mjengo wa kona za sehemu hii ya juu zitainuka kuliko sehemu nyingine.

16. Sehemu ya juu ya madhabahu itakuwa mraba, mita 6 kila upande.

17. Sehemu ya katikati, itakuwa mraba, sentimita 7 kila upande, nayo itakuwa na ukingo pembeni wenye kimo cha sentimita 25. Kutakuwa na mfereji wenye upana wa sentimita 50. Na kutakuwa na vidato vya kupandia madhabahu upande wa mashariki.

18. Bwana Mwenyezi-Mungu akaniambia: “Wewe mtu! Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Wakati madhabahu imejengwa, utaiweka wakfu kwa kutoa tambiko za kuteketezwa juu yake na kuinyunyizia damu ya wanyama waliotolewa sadaka.

19. Wale makuhani walio wa kabila la Lawi ambao ni wazawa wa Sadoki, ndio tu watakaonikaribia ili kunihudumia. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. Utawapa fahali mchanga kuwa sadaka ya kuondoa dhambi.

20. Utatwaa damu yake na kuitia juu ya pembe nne za madhabahu na juu ya ncha nne za daraja na juu ya pambizo yake pande zote. Hivyo ndivyo utakavyoitakasa madhabahu na kuiweka wakfu.

Ezekieli 43