3. Wao ni watu waasi. Basi, ewe mtu, fanya kama vile unakwenda uhamishoni: Ondoka wakiwa wanakuona, ukimbilie mahali pengine. Nenda kama mkimbizi kutoka mahali ulipo mpaka mahali pengine wao wakikuona. Labda wataelewa, ingawa wao ni waasi.
4. Hakikisha wanaona unachofanya. Funga mzigo wako uutoe nje na kuwa tayari kuondoka jioni kama wafanyavyo watu wanaokwenda uhamishoni.
5. Wakiwa wanakuangalia toboa ukuta wa nyumba, upitie hapo na kwenda nje.
6. Wakiwa wanakuona, jitwike mabegani mzigo wako na kuondoka wakati wa giza. Funika uso wako usiweze kuona unakwenda wapi. Ndivyo ninavyokufanya uwe ishara kwa Waisraeli.”
7. Basi, nikafanya kama nilivyoamriwa. Siku hiyo, wakati wa mchana, nikafunga mzigo wangu kama mzigo wa mtu anayekimbia. Jioni nikautoboa ukuta na giza lilipokuwa likiingia, nikatoka, nimejitwika mzigo wangu mabegani, watu wote wakiniona.