Danieli 11:11-26 Biblia Habari Njema (BHN)

11. Hapo, mfalme wa kusini, kwa hasira yake, atapigana vita na mfalme wa kaskazini ambaye naye atamkabili kwa jeshi kubwa, lakini litashindwa.

12. Baada ya kulishinda vibaya jeshi la kaskazini na kuua maelfu, ataanza kujisifu, ila hataendelea kuwa mshindi.

13. “ ‘Maana mfalme wa kaskazini baadaye ataandaa jeshi kubwa kuliko lile la awali. Kisha baada ya miaka kadhaa atarudi na jeshi kubwa lenye vifaa vingi.

14. Wakati huo watu wengi watamwasi mfalme wa kusini. Baadhi ya watu wakatili wa taifa lako Danieli, wataasi ili kutekeleza maono haya, lakini hawatafaulu.

15. Ndipo mfalme wa kaskazini atauzingira mji wenye ngome imara na kuuteka. Wanajeshi wa kusini hawatastahimili, hata wale wateule, maana hawatakuwa na nguvu.

16. Mvamizi atawatenda kama apendavyo, hakuna atakeyethubutu kupingana naye. Atasimama katika nchi tukufu, na nchi hiyo yote itakuwa chini ya mamlaka yake.

17. “ ‘Huyo mvamizi atakusudia kuja na jeshi lake lote, naye atafanya mapatano na kuyatekeleza. Atamwoza binti mmoja ili kuuangamiza ufalme wa adui yake; lakini mpango wake hautafaulu, wala kumfaidia lolote.

18. Baadaye, atazigeukia na kuzishambulia nchi nyingi za pwani na kuzishinda. Lakini jemadari mgeni atamshinda na kuyakomesha majivuno yake mwenyewe; naam, atamrudishia mfalme wa kaskazini majivuno yake mwenyewe.

19. Hapo atageuka kurudi katika ngome za nchi yake mwenyewe, lakini atajikwaa na kuanguka vitani na huo ndio utakaokuwa mwisho wake.

20. “ ‘Huyu atafuatwa na mfalme mwingine ambaye atatuma mtozaushuru kupitia katika fahari ya ufalme wake. Mfalme huyo atauawa baada ya siku chache, lakini si kwa hasira wala vitani.

21. “ ‘Mfalme atakayefuata atakuwa baradhuli ambaye hana idhini ya kushika ufalme, naye atakuja bila taarifa na kunyakua ufalme kwa hila.

22. Majeshi pamoja na kuhani wa hekalu, atawafagilia mbali na kuwaua.

23. Kwa kufanya mapatano, atayahadaa mataifa mengine, na ataendelea kupata nguvu ingawa atatawala taifa dogo.

24. Bila taarifa atazivamia sehemu za mkoa zenye utajiri mwingi na kufanya mambo ambayo hayakufanywa hata na mmoja wa wazee wake waliomtangulia. Kisha, atawagawia wafuasi wake mateka, mali na vitu alivyoteka nyara vitani. Atafanya mipango ya kuzishambulia ngome, lakini kwa muda tu.

25. “ ‘Kwa ujasiri mwingi, ataunda jeshi kubwa ili kuushambulia ufalme wa kusini, naye mfalme wa kusini atajibu mashambulizi hayo kwa jeshi kubwa zaidi na lenye nguvu sana. Lakini, mfalme wa kusini hatafaulu kwani mipango ya hila itafanywa dhidi yake.

26. Wale wanaokula pamoja naye, ndio watakaomwangamiza. Watamwangamiza na jeshi lake litafagiliwa mbali na wengi watauawa.

Danieli 11