2 Wakorintho 11:11-25 Biblia Habari Njema (BHN)

11. Kwa nini nasema hivyo? Kwa sababu eti siwapendi nyinyi? Mungu anajua kwamba nawapenda!

12. Nitaendelea kufanya kama ninavyofanya sasa, ili nisiwape nafasi wale wanaotafuta nafasi, nafasi ya kujivuna kwamba eti wanafanya kazi kama sisi.

13. Maana, hao ni mitume wa uongo, wafanyakazi wadanganyifu wanaojisingizia kuwa mitume wa Kristo.

14. Wala si ajabu, maana hata Shetani mwenyewe hujisingizia kuwa malaika wa mwanga!

15. Kwa hiyo si jambo la kushangaza ikiwa na hao watumishi wake wanajisingizia kuwa watumishi wa haki. Mwisho wao watapata kile wanachostahili kufuatana na matendo yao.

16. Tena nasema: Mtu asinifikirie kuwa mpumbavu. Lakini kama mkifikiri hivyo, basi, nichukueni kama mpumbavu ili nami nipate kuwa na cha kujivunia angaa kidogo.

17. Ninachosema sasa si kile alichoniagiza Bwana; kuhusu jambo hili la kujivuna, nasema tu kama mtu mpumbavu.

18. Maadamu wengi hujivuna kwa sababu za kidunia, nami pia nitajivuna.

19. Nyinyi ni wenye busara, ndiyo maana hata mnawavumilia wapumbavu!

20. Mnamvumilia hata mtu anayewafanya nyinyi watumwa, mtu mwenye kuwanyonya, mwenye kuwakandamiza, mwenye kuwadharau na kuwapiga usoni!

21. Kwa aibu nakubali kwamba sisi tulikuwa dhaifu.Iwe iwavyo, lakini kama kuna mtu yeyote anayethubutu kujivunia kitu – nasema kama mtu mpumbavu – mimi nathubutu pia.

22. Je, wao ni Waebrania? Hata mimi. Je, wao ni Waisraeli? Hata mimi. Wao ni wazawa wa Abrahamu? Hata mimi.

23. Wao ni watumishi wa Kristo? Hata mimi – nanena hayo kiwazimu – ni mtumishi wa Kristo zaidi kuliko wao. Mimi nimefanya kazi ngumu zaidi, nimekaa gerezani mara nyingi zaidi, nimepigwa mara nyingi zaidi na nimekaribia kifo mara nyingi.

24. Mara tano nilichapwa vile viboko arubaini kasoro kimoja vya Wayahudi.

25. Nilipigwa fimbo mara tatu, nilipigwa mawe mara moja; mara tatu nilivunjikiwa meli baharini, na humo nikakesha usiku kucha na kushinda mchana kutwa.

2 Wakorintho 11