2 Timotheo 2:15-26 Biblia Habari Njema (BHN)

15. Jitahidi kupata kibali kamili mbele ya Mungu kama mfanyakazi ambaye haoni haya juu ya kazi yake na ambaye hufundisha sawa ule ujumbe wa kweli.

16. Jiepushe na majadiliano yasiyofaa na ya kipumbavu; kwani hayo huzidi kuwatenga watu mbali na Mungu.

17. Mafundisho ya aina hiyo ni kama donda linalokula mwili. Miongoni mwa hao waliofundisha hayo ni Humenayo na Fileto.

18. Hawa wamepotoka kabisa mbali na ukweli, na wanatia imani ya watu wengine katika wasiwasi kwa kusema ati ufufuo wetu umekwisha fanyika.

19. Lakini msingi thabiti uliowekwa na Mungu uko imara, na juu yake yameandikwa maneno haya: “Bwana anawafahamu wale walio wake,” na “Kila asemaye yeye ni wa Bwana, ni lazima aachane na uovu.”

20. Katika nyumba kubwa kuna mabakuli na vyombo vya kila namna: Vingine ni vya fedha na dhahabu, vingine vya mbao na udongo, vingine vya matumizi ya heshima na vingine kwa ajili ya matumizi ya kawaida.

21. Basi, kama mtu atajitakasa kwa kujitenga mbali na mambo hayo yote maovu, atakuwa chombo cha matumizi ya pekee, kwa sababu amewekwa wakfu, anamfaa Bwana wake na yupo tayari kwa kila kazi njema.

22. Jiepushe na tamaa za ujana, fuata uadilifu, imani, upendo, amani, pamoja na watu wote ambao wanamwomba Bwana kwa moyo safi.

23. Epuka ubishi wa kijinga na kipumbavu; wajua kwamba hayo huleta magomvi.

24. Mtumishi wa Bwana asigombane. Anapaswa kuwa mpole kwa watu wote, mwalimu mwema na mvumilivu,

25. ambaye ni mpole anapowaonya wapinzani wake, kwani huenda Mungu akawajalia nafasi ya kutubu, wakapata kuujua ukweli.

26. Hapo fahamu zao zitawarudia tena, wakaponyoka katika mtego wa Ibilisi aliyewanasa na kuwafanya wayatii matakwa yake.

2 Timotheo 2