19. Pasaka hiyo iliadhimishwa katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wake mfalme Yosia.
20. Baada ya haya yote aliyofanya mfalme Yosia kwa ajili ya hekalu, Neko, mfalme wa Misri, aliongoza jeshi lake kwenda kushambulia Karkemishi kwenye mto Eufrate. Naye mfalme Yosia alitoka kumkabili,
21. lakini mfalme Neko akamtumia ujumbe usemao: “Vita hivi havikuhusu wewe hata kidogo ewe mfalme wa Yuda. Sikuja kupigana nawe bali dhidi ya maadui zangu, na Mungu ameniamuru niharakishe. Acha basi kumpinga Mungu, ambaye yu upande wangu, la sivyo atakuangamiza.”
22. Lakini Yosia hakukubali kumwachia. Alikataa kuyasikiliza maneno aliyonena Mungu kwa njia ya Neko, kwa hiyo akajibadilisha ili asitambulike, kisha akaingia vitani katika tambarare ya Megido.
23. Nao wapiga upinde walimpiga mshale mfalme Yosia; basi ndipo mfalme alipowaambia watumishi wake: “Niondoeni! Nimejeruhiwa vibaya sana.”