26. Adui wa mwisho atakayeangamizwa ni kifo.
27. Maana, Maandiko yasema: “Mungu ameweka vitu vyote chini ya miguu yake.” Lakini, Maandiko yanaposema: “Vitu vyote vimewekwa chini ya miguu yake avitawale” ni dhahiri kwamba Mungu haingii katika kundi hilo la vitu, maana yeye ndiye anayeviweka vitu hivyo chini ya Kristo.
28. Lakini vitu vyote vitakapowekwa chini ya utawala wa Kristo, ndipo naye Mwana atakapojiweka chini ya Mungu, aliyeweka vyote chini ya utawala wake; ili Mungu atawale juu ya vyote.
29. Kama hakuna ufufuo, je watu wale wanaobatizwa kwa ajili ya wafu wanatumainia kupata nini? Kama wafu hawafufuliwi, ya nini kubatizwa kwa ajili yao?
30. Na sisi, ya nini kujitia hatarini kila saa?
31. Ndugu, mimi nakikabili kifo kila siku! Fahari niliyo nayo juu yenu katika kuungana na Kristo Yesu Bwana wetu inanifanya nitangaze jambo hili.
32. Kama kusudi langu lingalikuwa la kibinadamu tu, kule kupigana kwangu na wanyama wakali hapa Efeso kungalinifaa kitu gani? Kama wafu hawafufuki, basi, “Tule na tunywe, maana kesho tutakufa.”
33. Msidanganyike! Urafiki mbaya huharibu tabia njema.