1 Wafalme 7:17-30 Biblia Habari Njema (BHN)

17. Halafu, alifuma nyavu mbili zenye mapambo ya mrabamraba, akatengeneza na taji kwa kusokota mkufu: Vyote hivyo kwa ajili ya kupamba taji za shaba zilizowekwa juu ya zile nguzo.

18. Hali kadhalika, alitengeneza matunda aina ya makomamanga, akayapanga safu mbili kuzunguka zile taji juu ya kila nguzo.

19. Na taji hizo zilizokuwa juu ya nguzo mbele ya sebule, zilipambwa kwa mifano ya maua ya yungiyungi, kimo chake mita 1.75.

20. Taji hizo zilikuwa juu ya hizo nguzo mbili, na pia zilikuwa juu ya sehemu ya mviringo iliyojitokeza karibu na zile nyavu. Palikuwa na mifano 400 ya matunda ya mkomamanga, imepangwa safu mbili kuzunguka kila taji.

21. Hiramu aliziweka nguzo hizo kwenye sebule ya hekalu; nguzo aliyoisimika upande wa kusini iliitwa Yakini, na ile aliyoisimika upande wa kaskazini iliitwa Boazi.

22. Vichwa vya nguzo hizo vilipambwa kwa mfano wa maua ya yungiyungi. Na hivyo kazi ya kutengeneza nguzo ikamalizika.

23. Hiramu alitengeneza Birika liitwalo Bahari. Lilikuwa la mviringo lenye upana wa mita 4.5 kutoka ukingo hadi ukingo, na urefu wa mita 2.25 na mzingo wa mita 13.5.

24. Chini ya ukingo wake, kulizunguka tangi hilo, kulikuwa na safu mbili za vibuyu, kila kimoja mita 13.5. Vibuyu hivyo vilikuwa vimetengenezwa wakati huohuo tangi hilo lilipofanywa.

25. Nalo tangi lilikuwa limewekwa juu ya sanamu za mafahali kumi na wawili; tatu zikielekea upande wa kaskazini, tatu zikielekea magharibi, tatu kusini, na nyingine tatu mashariki. Tangi liliwekwa juu ya mafahali hao, sehemu zao za nyuma zikiwa ndani.

26. Unene wa ukingo wake ulikuwa sentimita 7.5; nao ulikuwa ukifanana na ukingo wa kikombe na kama ua la yungiyungi. Tangi liliweza kujaa maji kiasi cha lita 40,000.

27. Hiramu pia alitengeneza magari kumi ya shaba, kila gari likiwa na urefu wa mita 1.75, upana wa mita 1.75, na kimo cha mita 1.25.

28. Magari hayo yalikuwa yameundwa hivi: Kulikuwa na mabamba ya chuma ambayo yalikuwa yameshikiliwa na mitalimbo. Juu ya mabamba hayo yaliyoshikiliwa na mitalimbo,

29. kulikuwa na sanamu za simba, mafahali na viumbe wenye mabawa. Sanamu hizo za simba na mafahali, zilikuwa zimefunikwa na kutandikwa mapambo yaliyosokotwa vizuri.

30. Isitoshe, kila gari lilikuwa na magurudumu manne ya shaba, na vyuma vya katikati vya kuyazungukia magurudumu hayo, vilikuwa vya shaba. Kwenye pembe nne za gari kulikuwa na vishikizo vya shaba kwa ajili ya birika kubwa. Karibu ya kila kishikio kuliwekwa mapambo ya maua ya kusokotwa.

1 Wafalme 7