1 Samueli 25:39-44 Biblia Habari Njema (BHN)

39. Daudi aliposikia kwamba Nabali amekufa, alisema, “Atukuzwe Mwenyezi-Mungu ambaye amemlipiza kisasi Nabali kwa kunitukana, naye Mwenyezi-Mungu ameniepusha mimi mtumishi wake kutenda maovu. Mwenyezi-Mungu amempatiliza Nabali kwa uovu wake.” Kisha Daudi alituma watu ili wamposee Abigaili awe mke wake.

40. Watumishi wa Daudi walipowasili kwa Abigaili huko Karmeli, wakamwambia, “Daudi ametutuma kukuchukua ili uwe mke wake.”

41. Abigaili aliinuka, na kuinama mbele yao mpaka chini, akasema, “Mimi ni mtumishi tu; niko tayari kuosha miguu ya watumishi wa bwana wangu.”

42. Abigaili alifanya haraka, akainuka na kupanda juu ya punda wake, akifuatana na watumishi wake wa kike watano, akaenda na watumishi wa Daudi; naye akawa mke wa Daudi.

43. Tena Daudi alimwoa Ahinoamu kutoka Yezreeli. Hivyo hao wawili wakawa wake zake.

44. Wakati huo, Shauli alikuwa amemwoza binti yake Mikali, ambaye alikuwa mke wa Daudi, kwa Palti mwana wa Laishi, kutoka mji wa Galimu.

1 Samueli 25