1 Samueli 2:16-25 Biblia Habari Njema (BHN)

16. Na kama mtu huyo akimjibu, “Ngojea kwanza nichome mafuta halafu utachukua kiasi chochote unachotaka,” hapo huyo mtumishi wa kuhani humjibu, “La, ni lazima unipe sasa hivi. La sivyo, nitaichukua kwa nguvu.”

17. Dhambi hii ya vijana hao wa Eli ilikuwa kubwa sana mbele ya Mwenyezi-Mungu. Maana, vijana hao walidharau matoleo ya Mwenyezi-Mungu.

18. Wakati huo, kijana Samueli aliendelea kumtumikia Mwenyezi-Mungu, akiwa amevaa kizibao cha kitani.

19. Kila mwaka mama yake alimfumia vazi dogo, na kumpelekea alipokuwa akienda na mumewe kutolea tambiko ya kila mwaka.

20. Eli aliwabariki Elkana na mkewe, akisema, “Mwenyezi-Mungu na akupe wewe Elkana watoto wengine kwa mwanamke huyu ili wachukue mahali pa yule uliyempa Mwenyezi-Mungu.” Kisha wao hurudi nyumbani.

21. Mwenyezi-Mungu alimhurumia Hana naye akajaliwa kupata watoto wa kiume watatu na mabinti wawili. Mtoto Samueli akaendelea kukua mbele ya Mwenyezi-Mungu.

22. Wakati huo Eli alikuwa mzee sana. Aliposikia yote ambayo watoto wake wa kiume walikuwa wanawatendea Waisraeli, jinsi walivyokuwa wanalala na wanawake waliokuwa wanahudumu kwenye mlango wa hema la mkutano,

23. aliwauliza, “Kwa nini mnafanya mambo haya? Nasikia kutoka kwa watu wote juu ya maovu mnayoyafanya.

24. Msifanye hivyo wanangu kwa sababu mambo hayo ninayoyasikia kutoka kwa watu wa Mwenyezi-Mungu ni mabaya.

25. Mtu akimkosea mwenzake, anaweza kuombewa kwa Mungu, ili Mungu amsamehe. Lakini mtu akimkosea Mwenyezi-Mungu nani awezaye kumwombea msamaha?” Lakini watoto hao hawakumsikiliza baba yao, kwani Mwenyezi-Mungu alikwisha kata shauri kuwaua.

1 Samueli 2