1 Samueli 16:5-10 Biblia Habari Njema (BHN)

5. Samueli akawaambia, “Nimekuja kwa amani. Nimekuja kumtolea tambiko Mwenyezi-Mungu. Jitakaseni wenyewe halafu twendeni kutoa tambiko.” Samueli akamtakasa Yese pamoja na wanawe, akawakaribisha kwenye tambiko.

6. Walipofika, na Samueli alipomwona Eliabu, alijisemea moyoni mwake, “Hakika, mpakwa mafuta wa Mwenyezi-Mungu ndiye huyu aliye mbele ya Mwenyezi-Mungu!”

7. Lakini Mwenyezi-Mungu alimwambia, “Usiangalie sura yake na urefu wa kimo chake. Mimi nimemkataa kwani siangalii mambo kama wanavyoyaangalia binadamu wenye kufa. Binadamu huangalia uzuri wa nje, lakini mimi naangalia moyoni.”

8. Kisha, Yese akamwita Abinadabu na kumleta mbele ya Samueli. Lakini Samueli akasema, “Wala huyu hakuchaguliwa na Mwenyezi-Mungu.”

9. Yese akamleta Shama. Samueli akasema, “Wala huyu hakuchaguliwa na Mwenyezi-Mungu.”

10. Yese aliwapitisha wanawe wote saba mbele ya Samueli lakini Samueli akamwambia, “Mwenyezi-Mungu hajamchagua yeyote kati ya hawa.”

1 Samueli 16