111. Shuhuda zako nimezifanya urithi wa milele,Maana ndizo changamko la moyo wangu.
112. Nimeuelekeza moyo wangu nizitende amri zako,Daima, naam, hata milele.
113. Watu wa kusita-sita nawachukia,Lakini sheria yako naipenda.
114. Ndiwe sitara yangu na ngao yangu,Neno lako nimelingojea.
115. Enyi watenda mabaya, ondokeni kwangu,Niyashike maagizo ya Mungu wangu.
116. Unitegemeze sawasawa na ahadi yako, nikaishi,Wala usiniache niyaaibikie matumaini yangu.
117. Unisaidie nami nitakuwa salama,Nami nitaziangalia amri zako daima.
118. Umewakataa wote wazikosao amri zako,Kwa maana hila zao ni uongo.
119. Wabaya wa nchi pia umewaondoa kama takataka,Ndiyo maana nimezipenda shuhuda zako.
120. Mwili wangu unatetemeka kwa kukucha Wewe,Nami ninaziogopa hukumu zako.
121. Nimefanya hukumu na haki,Usiniache mikononi mwao wanaonionea.
122. Uwe mdhamini wa mtumishi wako, apate mema,Wenye kiburi wasinionee.
123. Macho yangu yamefifia kwa kuutamani wokovu wako,Na ahadi ya haki yako.
124. Kama zilivyo rehema zako umtendee mtumishi wako,Na amri zako unifundishe.
125. Mimi ni mtumishi wako, unifahamishe,Nipate kuzijua shuhuda zako.
126. Wakati umewadia BWANA atende kazi;Kwa kuwa wameitangua sheria yako.
127. Ndiyo maana nimeyapenda maagizo yako,Kuliko dhahabu, naam, dhahabu iliyo safi.
128. Maana nayaona mausia yako yote kuwa ya adili,Kila njia ya uongo naichukia.