14. Huyo Kalebu aliwafukuza watoke hapo hao wana watatu wa Anaki, nao ni Sheshai, na Ahimani, na Talmai, wana wa Anaki.
15. Kisha akakwea kutoka huko ili kuwaendea wenyeji wa Debiri; jina la Debiri hapo kwanza lilikuwa Kiriath-seferi.
16. Kalebu akasema, Yeye atakayeupiga Kiriath-seferi na kuutwaa, mimi nitampa Aksa binti yangu awe mkewe.
17. Naye Othnieli mwana wa Kenazi, nduguye Kalebu, aliutwaa; basi akampa Aksa binti yake awe mkewe.
18. Kisha ikawa, hapo huyo mwanamke alipokwenda kwa mumewe, akamtaka aombe shamba kwa baba yake; akashuka katika punda wake; Kalebu akamwuliza, Wataka nini?