Yer. 51:32-41 Swahili Union Version (SUV)

32. Navyo vivuko vimeshambuliwa,Nayo makangaga wameyatia moto,Nao watu wa vita wameingiwa na hofu.

33. Kwa maana BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi; Binti Babeli amekuwa kama sakafu ya kufikichia wakati wa kukanyagwa kwake; bado kitambo kidogo na wakati wa mavuno utafika kwake.

34. Nebukadreza, mfalme wa Babeli, amenila, ameniseta, amenifanya kuwa chombo kitupu; amenimeza kama joka, amelijaza tumbo lake vitu vyangu vya anasa; amenitupa

35. Udhalimu niliotendwa mimi, na uliotendwa mwili wangu, umpate Babeli; ndivyo atakavyosema yeye akaaye Sayuni; na Yerusalemu atasema, Damu yangu na iwe juu yao wakaao katika Ukaldayo.

36. Basi, BWANA asema hivi, Tazama, nitakutetea, nami nitatwaa kisasi kwa ajili yako; nami nitaikausha bahari yake, nitaifanya chemchemi yake kuwa pakavu.

37. Na Babeli utakuwa magofu, makao ya mbwa-mwitu, ajabu, na mazomeo, pasipo mtu wa kukaa huko.

38. Watanguruma pamoja kama wana-simba; watanguruma kama simba wachanga.

39. Wakiingiwa na ukali, nitawafanyizia karamu yao, nami nitawalevya, wapate kufurahi, na kulala usingizi wa milele, wasiamke tena, asema BWANA.

40. Nitawatelemsha kama wana-kondoo machinjoni, kama kondoo waume pamoja na mabeberu.

41. Jinsi Sheshaki alivyotwaliwa!Naye sifa ya dunia yote alivyoshambuliwa!Jinsi Babeli alivyokuwa ukiwaKatikati ya mataifa!

Yer. 51