Yer. 49:20-39 Swahili Union Version (SUV)

20. Basi, lisikieni shauri la BWANA;Alilolifanya juu ya Edomu;Na makusudi yake aliyoyakusudiaJuu yao wakaao Temani;Hakika watawaburura, naam, wadogo wa kundi;Hakika malisho yao yatafadhaika kwa ajili yao.

21. Nchi yatetemeka kwa sauti ya kuanguka kwao;Kuna kilio, sauti yake yasikiwa katika Bahari ya Shamu.

22. Tazama, atapanda na kuruka kama tai, na kutandaza mabawa yake juu ya Bozra; na mioyo ya mashujaa wa Edomu siku hiyo itakuwa kama moyo wa mwanamke katika utungu wake.

23. Habari za Dameski.Hamathi umetahayarika, na Arpadi pia;Maana wamesikia habari mbaya;Wameyeyuka kabisa;Huzuni iko baharini, haiwezi kutulia.

24. Dameski umedhoofika;Umejigeuza kukimbia; tetemko limeushika;Dhiki na huzuni zimeupata,Kama za mwanamke katika utungu wake.

25. Imekuwaje mji wa sifa haukuachwa, mji wa furaha yangu?

26. Kwa hiyo vijana wake wataanguka katika njia kuu zake, na watu wote wa vita watanyamazishwa katika siku hiyo, asema BWANA wa majeshi.

27. Nami nitawasha moto katika ukuta wa Dameski, nao utayateketeza majumba ya Ben-hadadi.

28. Habari za Kedari, na za falme za Hazori, ambazo Nebukadreza, mfalme wa Babeli, alizipiga. BWANA asema hivi, Ondokeni, pandeni hata Kedari, mkawateke nyara wana wa mashariki.

29. Hema zao na makundi yao watayatwaa; watachukulia mbali mapazia yao kwa faida yao wenyewe, na vyombo vyao vyote, na ngamia zao; nao watawapigia kelele wakisema, Hofu ziko pande zote.

30. Kimbieni ninyi, enendeni mbali mkitanga-tanga, kaeni chini sana, enyi mkaao Hazori, asema BWANA; maana Nebukadreza, mfalme wa Babeli, amefanya shauri juu yenu, naye amekusudia neno juu yenu.

31. Ondokeni, pandeni hata taifa lililo katika hali ya raha, likaalo bila kuhangaika, asema BWANA; wasio na malango wala makomeo, wakaao peke yao.

32. Na ngamia zao watakuwa mateka, na wingi wa makundi yao utakuwa nyara; nami nitawatawanya hata pepo zote watu wale wanyoao denge; nami nitaleta msiba wao toka pande zao zote, asema BWANA.

33. Na Hazori utakuwa kao la mbwa-mwitu; ukiwa milele; hapana mtu atakayekaa huko, wala hapana mwanadamu atakayekaa huko kama mgeni akaavyo.

34. Neno la BWANA lililomjia Yeremia, nabii, juu ya Elamu, mwanzo wa kumiliki kwake Sedekia, mfalme wa Yuda, kusema,

35. BWANA wa majeshi asema hivi, Tazama nitauvunja upinde wa Elamu, ulio mkuu katika nguvu zao.

36. Na juu ya Elamu nitazileta pepo nne, toka pembe nne za mbinguni, nami nitawatawanya hata pepo nne zote, wala hapana taifa ambalo hawatalifikilia watu wa Elamu waliofukuzwa.

37. Nami nitawafadhaisha watu wa Elamu mbele ya adui zao, na mbele ya hao wanaowatafuta roho zao; nami nitawaletea mabaya, naam, hasira yangu kali, asema BWANA; nami nitautuma upanga uwafuatie, hata nitakapowaangamiza;

38. nami nitaweka kiti changu cha enzi huko Elamu, nami nitawaharibu, mfalme na wakuu, watoke huko, asema BWANA.

39. Lakini itakuwa, katika siku za mwisho, nitawarudisha wafungwa wa Elamu, asema BWANA.

Yer. 49