7. Kwa hiyo, angalia, siku zinakuja, asema BWANA, ambapo hawatasema tena, Aishivyo BWANA, aliyewatoa wana wa Israeli katika nchi ya Misri;
8. lakini, Aishivyo BWANA, aliyewapandisha na kuwaongoza wazao wa nyumba ya Israeli kutoka nchi ya kaskazini, na kutoka nchi zote nilikowafukuza; nao watakaa katika nchi yao wenyewe.
9. Katika habari za manabii.Moyo wangu ndani yangu umevunjika,Mifupa yangu yote inatikisika.Nimekuwa kama mtu aliye mlevi,Na kama mtu aliyeshindwa na divai;kwa ajili ya BWANA, na kwa ajili ya maneno yake matakatifu.
10. Maana nchi imejaa wazinzi; kwa sababu ya kuapa nchi inaomboleza; malisho ya nyikani yamekauka; mwenendo wao ni mbaya, na nguvu zao si za haki.
11. Maana nabii, na kuhani, wote wawili wanakufuru; naam, katika nyumba yangu nimeuona uovu wao, asema BWANA.
12. Kwa ajili ya hayo njia yao itakuwa kwao kama mahali pa kuteleza gizani; watatelemshwa na kuanguka hapo; kwa maana nitaleta uovu juu yao, naam, mwaka wa kujiliwa kwao, asema BWANA.
13. Nami nimeona upumbavu katika manabii wa Samaria; walitabiri kwa Baali, wakawakosesha watu wangu Israeli.
14. Katika manabii wa Yerusalemu nimeona neno linalochukiza sana; hufanya zinaa; huenenda katika maneno ya uongo, hutia nguvu mikono ya watendao maovu, hata ikawa hapana mtu arejeaye na kuuacha uovu wake; wote pia wamekuwa kama Sodoma kwangu, na wenyeji wake kama Gomora.
15. Basi BWANA wa majeshi asema hivi, katika habari ya manabii, Tazama, nitawalisha pakanga, nitawanywesha maji ya uchungu; kwa kuwa kutoka kwa manabii hao wa Yerusalemu kukufuru kumeingia katika nchi yote.
16. BWANA wa majeshi asema hivi, Msisikilize maneno ya manabii wakiwatabiria; huwafundisha ubatili; hunena maono ya mioyo yao wenyewe; hayakutoka katika kinywa cha BWANA.
17. Daima huwaambia wao wanaonidharau, BWANA amesema, Mtakuwa na amani; nao humwambia kila mtu aendaye kwa ukaidi wa moyo wake, Hamtapatwa na ubaya wo wote.