4. watakufa kwa maradhi mabaya; hawataliliwa, wala hawatazikwa; watakuwa kama samadi juu ya uso wa nchi; nao wataangamizwa kwa upanga, na kwa njaa; na mizoga yao itakuwa chakula cha ndege wa angani, na cha wanyama wa nchi.
5. Maana BWANA asema hivi, Usiingie ndani ya nyumba yenye matanga, wala usiende kuwaombolezea, wala kuwalilia; maana nimewaondolea watu hawa amani yangu, asema BWANA, hata fadhili zangu na rehema zangu.
6. Wakubwa kwa wadogo wote pia watakufa katika nchi hii; hawatazikwa, wala watu hawatawalilia, wala kujikata-kata kwa ajili yao, wala kujinyoa kwa ajili yao;
7. wala watu hawatamega mkate kwa ajili yao, wakati wa kuomboleza, ili kuwafariji kwa ajili yao waliokufa; wala watu hawatawapa kikombe cha faraja, wanywe kwa ajili ya baba yao au mama yao.
8. Wala usiingie ndani katika nyumba yenye karamu, kuketi pamoja nao, na kula na kunywa.