1. Ndugu zangu, hamjui (maana nasema na hao waijuao sheria) ya kuwa torati humtawala mtu wakati anapokuwa yu hai?
2. Kwa maana mwanamke aliye na mume amefungwa na sheria kwa yule mume wakati anapokuwa yu hai; bali akifa yule mume, amefunguliwa ile sheria ya mume.
3. Basi wakati awapo hai mumewe, kama akiwa na mume mwingine huitwa mzinzi. Ila mumewe akifa, amekuwa huru, hafungwi na sheria hiyo, hata yeye si mzinzi, ajapoolewa na mume mwingine.
4. Kadhalika, ndugu zangu, ninyi pia mmeifia torati, kwa njia ya mwili wa Kristo, mpate kuwa mali ya mwingine, yeye aliyefufuka katika wafu, kusudi tumzalie Mungu matunda.
5. Kwa maana tulipokuwa katika hali ya mwili, tamaa za dhambi, zilizokuwako kwa sababu ya torati, zilitenda kazi katika viungo vyetu hata mkaizalia mauti mazao.