Mt. 27:5-18 Swahili Union Version (SUV)

5. Akavitupa vile vipande vya fedha katika hekalu, akaondoka; akaenda, akajinyonga.

6. Wakuu wa makuhani wakavitwaa vile vipande vya fedha, wakasema, Si halali kuviweka katika sanduku ya sadaka, kwa kuwa ni kima cha damu.

7. Wakafanya shauri, wakavitumia kwa kununua konde la mfinyanzi liwe mahali pa kuzika wageni.

8. Kwa hiyo konde lile huitwa konde la damu hata leo.

9. Ndipo likatimia neno lililonenwa na nabii Yeremia, akisema, Wakavitwaa vipande thelathini vya fedha, kima chake aliyetiwa kima, ambaye baadhi ya Waisraeli walimtia kima;

10. wakavitumia kwa kununua konde la mfinyanzi, kama Bwana alivyoniagiza.

11. Naye Yesu akasimama mbele ya liwali; liwali akamwuliza, akasema, Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi? Yesu akamwambia, Wewe wasema.

12. Lakini aliposhitakiwa na wakuu wa makuhani na wazee, hakujibu hata neno.

13. Ndipo Pilato akamwambia, Husikii ni mambo mangapi wanayokushuhudia?

14. Asimjibu hata neno moja, hata liwali akastaajabu sana.

15. Basi wakati wa siku kuu, liwali desturi yake huwafungulia mkutano mfungwa mmoja waliyemtaka.

16. Basi palikuwa na mfungwa mashuhuri siku zile, aitwaye Baraba.

17. Basi walipokutanika, Pilato akawaambia, Mnataka niwafungulie yupi? Yule Baraba, au Yesu aitwaye Kristo?

18. Kwa maana alijua ya kuwa wamemtoa kwa husuda.

Mt. 27