34. Hayo yote Yesu aliwaambia makutano kwa mifano; wala pasipo mfano hakuwaambia neno;
35. ili litimie neno lililonenwa na nabii, akisema,Nitafumbua kinywa changu kwa mifano,Nitayatamka yaliyositirika tangu awali.
36. Kisha Yesu akawaaga makutano, akaingia nyumbani; wanafunzi wake wakamwendea, wakasema, Tufafanulie mfano wa magugu ya kondeni.
37. Akajibu, akasema, Azipandaye zile mbegu njema ni Mwana wa Adamu;
38. lile konde ni ulimwengu; zile mbegu njema ni wana wa ufalme; na yale magugu ni wana wa yule mwovu;
39. yule adui aliyeyapanda ni Ibilisi; mavuno ni mwisho wa dunia; na wale wavunao ni malaika.
40. Basi, kama vile magugu yakusanywavyo na kuchomwa motoni; ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia.