2. Basi Mafarisayo wakamwendea, wakamwuliza, Je! Ni halali mtu kumwacha mkewe? Huku wakimjaribu.
3. Naye akajibu, akawaambia, Musa aliwaamuru nini?
4. Wakasema, Musa alitoa ruhusa kuandika hati ya talaka na kumwacha.
5. Yesu akawaambia, Kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu aliwaandikia amri hii.
6. Lakini tangu mwanzo wa kuumbwa ulimwengu, aliwafanya mume na mke.
7. Kwa sababu hiyo mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe;
8. na hao wawili watakuwa mwili mmoja; hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja.
9. Basi alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe.
10. Hata nyumbani tena wanafunzi wakamwuliza habari ya neno hilo.
11. Akawaambia, Kila mtu atakayemwacha mkewe na kuoa mwingine azini juu yake;
12. na mke, akimwacha mumewe na kuolewa na mtu mwingine, azini.
13. Basi wakamletea watoto wadogo ili awaguse; wanafunzi wake wakawakemea.
14. Ila Yesu alipoona alichukizwa sana, akawaambia, Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie; kwa maana watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao.